The United Republic of Tanzania
ARUSHA TECHNICAL COLLEGE
Skills make the difference
Post Details
WABUNIFU WACHANGA CHUO CHA UFUNDI ARUSHA KUENDELEZWA KUPITIA MIRADI YA BENKI YA DUNIA
Benki ya Dunia imedhamiria kuendelea kuwainua wabunifu wachanga wanaozalishwa kupitia vyuo vya kati katika nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe ili waweze kutimiza ndoto zao na kuweza kujikwamua kwenye wimbi la umasikini lililogubika nchi nyingi za Afrika. Miongoni mwa vyuo vya kati vitakavyonufaika na fursa hiyo ni Chuo cha Ufundi Arusha ambacho kimekua kikiibua wabunifu wengi katika fani mbalimbali za ufundi ambao wengi wao wamejiajiri na wengine kuajiriwa kwenye sekta binafsi na za umma. Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bw. Nathan Belete alipokuwa Chuo cha Ufundi Arusha kufungua na kushiriki mkutano ulioendeshwa kwa njia ya mtandao kati ya vyuo vya kati vilivyopo katika nchi za Tanzania, Malawi Zambia na Zimbabwe kujadili fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia ubunifu. “Leo tumekutanisha pamoja vijana kutoka nchi nne kujadili mambo muhimu wanayohitaji katika kuendeleza fani zao na kuangalia sehemu ambazo wanaweza kupata maarifa na kujiongezea kipato, Katika nchi ya Tanzania Benki ya Dunia inasaidia Zaidi ya dola za kimarekani 1.5 za uwekezaji katika miradi mbalimbali ya elimu yenye lengo la kunyanyua elimu ya Tanzania” alieleza Bw. Belete. Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Musa Chacha ameeleza kwamba Chuo hicho tangu awali kinatekeleza sera ya serikali ya kuandaa wabunifu wenye ujuzi wa vitendo na kwa kuanzia imeshaanza kuandaa kiwanda kidogo kitakachotumika kuzalisha kupitia wanafunzi wanaosoma hapo. “Kama Chuo tunatekeleza sera ya elimu kwa vitendo, kuna kiwanda kidogo ambacho tunakiandaa sasa hivi na kimeshafika hatua nzuri ili kikamilike ambacho wanafunzi wakiwa wanaingia hapa Chuoni watakua wanaajiriwa katika hicho kiwanda kwa muda ule ambao wanasoma, nia ya kiwanda hicho ni kuzalisha vitu vidogo vidogo vinavyoletwa kutoka nchi za nje kama vile vitasa vya milango, bawaba na makomeo” alisema Dkt. Chacha. Vilevile aliongeza “Pia tunajenga hospitali yetu hapa chuoni ambayo pamoja na matibabu mazuri yatakayotolewa, tunatarajia kuanza kutengeneza vifaa vidogovidogo vya matibabu kama vile kifaa cha kupima msukumo wa damu (BP) na vingine vingi”.
Other Posts